29/01/2011 10.28.35


Familia za kikristo zina dhamana ya kukuza na kulea miito mitakatifu ndani ya Kanisa


|

Familia za kikristo ni chimbuko la miito mitakatifu ndani ya Kanisa, hili ndilo Kanisa la nyumbani, shule ya utakatifu, haki, amani, upendo na ukarimu. Ni mahali ambapo mtu anajifunza kuonja upendo na hali ya kujitoa kwa ajili ya wengine, changamoto kwa wazazi kuwa kweli ni mashahidi wa tunu msingi za maisha ya kifamilia.
Mheshimiwa Padre Solomon Bandiho, Gombera wa Seminari kuu ya Kipalapala, Tabora anasema, familia inaweza kuleta msukumo wa pekee katika kukua na kuongezeka kwa miito mitakatifu kwa njia ya ushuhuda wa maisha ya sala, ushiriki mkamilifu katika Sakramenti za Kanisa, usomaji na tafakari ya Neno la Mungu ndani ya familia, pamoja na jitihada za kulimwilisha Neno la Mungu liweze kuwa ni dira katika maisha ya kifamilia. Kwa njia hii, watoto tangu mwanzo wanapata hamu na ari ya kumfahamu Kristo na Kanisa lake, hata kuwa tayari kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya maisha ya kipadre na kitawa.
Ili kuweza kufikia azma hii nyeti, Padre Bandiho anasema, kuna haja kwa familia kujitahidi kuwa na muda kwa ajili ya watoto wao, ili kujenga ari na mwamko wa kufahamiana zaidi pamoja na kushirikisha masuala muhimu ya maisha. Anakumbusha kwamba, wingi wa miito ni dhamana shirikishi inayojikita pia katika familia, hasa zaidi kwa njia ya ushuhuda kutoka ndani ya familia yenyewe.
Familia zina wajibu wa kulea miito mitakatifu, ili kupata wahudumu wa Injili: watakatifu, wachamungu na wadumifu katika wito na maisha yao.
|