26/01/2011 11.23.20


DRC: Iweni waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya ushuhuda wa maisha!


|

Waamini wa Jimbo Katoliki la Bunia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo, wanaelekea kufunga maadhimisho ya Jubilee ya miaka mia moja tangu waliposikia kwa mara ya kwanza, Habari Njema ya Wokovu ikitangazwa masikioni mwao. Kipindi cha mwaka mzima, imekuwa ni fursa kwa waamini kuonja kwa mara nyingine tena neema ya Mungu katika hija ya maisha yao ya kikristo, kwa kuweza kuipokea na kuitunza zawadi ya imani kwa kipindi cha miaka mia moja, changamoto iliyoko mbele yao kwa sasa ni kuendelea kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, kwa njia ya ushuhuda wa maisha.
Askofu Dieudonne Uringi wa Jimbo la Bunia anasema, zawadi ya Injili ya Kristo Jimboni mwao ililetwa na Shirika la Wamissionari wa Afrika na sasa inaendelea kuzaa matunda ya wongofu na utakatifu wa maisha miongoni mwa wafuasi wa Kristo. Maadhimisho ya Jubilee ya miaka mia moja ya Ukristo Jimbo Katoliki Bunia, umekuwa ni muda wa kufanya tafakari na tathmini ya kina kuhusu mikakati ya kichungaji, mafundisho na katekesi, mbinu na mikakati mipya katika Uinjilishaji wa kina, unaopania kugusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.
Waamini kwa ujumla wamepata nafasi pia ya kuangalia mchango wa Kanisa Katoliki Jimbo la Bunia katika huduma ya elimu na afya, wakipania kuboresha huduma hizi kama njia ya kumhudumia mtu mzima kiroho na kimwili. Kwa namna ya pekee, waamini walei, wanaalikwa kuwa ni wahudumu wakuu wa zawadi ya maisha, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa Mama yake hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Wamechangamotishwa kukataa katu katu kukumbatia utamaduni wa kifo unaoanza kupenyezwa kwa sera za utoaji mimba kama shinikizo la kupata misaada ya kiutu kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa.
Waamini wanapaswa kujikita zaidi katika maisha ya Kisakramenti, yanayowapatia nguvu ya kuweza kusonga mbele kwa imani, matumaini na mapendo, wanapotolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Familia zinaendelea kukumbushwa kwamba, ni kiini na chimbuko la miito mitakatifu ndani ya Kanisa, hivyo, wanapaswa kutekeleza wajibu wao kikamilifu badala ya kuviachia vyombo vya habari kuifanya kazi hii nyeti ya malezi.
Jitihada za majadiliano ya kiekumene zinaendelea kuzaa matunda kwa wakati wake, lakini kinachoshangaza kwa sasa ni mfumuko wa Makanisa ya Kikristo, jambo linaloleta changamoto ya kuwa makini katika mafundisho ya Kanisa, Imani ya Kanisa Katoliki na Kweli za Kiinjili, vinginevyo wakatoliki wanaweza kujikuta wakisombwa na wimbi la mafundisho mepesi mepesi yanayopania kuwaonjesha miujiza ya Kristo pamoja na kuwapatia ufumbuzi wa matatizo yao hasa kuhusu ukata na hali ngumu ya maisha.
Kanisa Katoliki DRC bado linachangamotishwa kuwa ni chombo cha upatanisho, haki na amani, sanjari na kukabiliana na mmong’onyoko wa tunu msingi za kiutu na kimaadili. Ili kukabiliana na changamoto hizi, Jimbo Katoliki la Bunia limeunda kamati maalum ya kichungaji, itakayobaini na kutafuta mbinu mkakati wa kukabiliana nazo.
Jimbo Katoliki la Bunia lilianzishwa kunako mwaka 1911 na kilele cha Jubilee ya miaka mia moja hi hapo tarehe 28 Januari, 2011 Ibada inayotarajiwa kufanyika kwenye Kanisa kuu la Jimbo la Bunia, DRC. Hili ni Jimbo linalojivunia wingi wa miito ya kipadre na kitawa kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa nchini DRC.
|