10/01/2011 10.01.29


Mafundisho Jamii ya Kanisa ni Biblia ya Kiafrika katika mchakato wa kudumisha haki, amani na mafao ya wengi ndani ya jamii


|

Katika makala yaliyotangulia tulitafakari kuhusu endelevu ya mafundisho ya kanisa, na kwamba yanafaa katika mazingira yote, tamaduni zote na kwa nyakati zote. Kumbe leo tutatafakari mafundisho hayo kwa nyakati zetu tukisaidiwa na maelezo ya historia. Historia inatueleza kwamba neno “mafundisho ya jamii” limeanza kuzungumzwa na Papa Pius XI (katika barua yake ya mwaka 1931 – “Quadragesimo Anno” - Miaka 40 baada ya barua ya Papa Leo XIII - “Rerum Novarum” “Mambo Mapya” ya mwaka 1891), kama mkusanyiko wa mafundisho kuhusu masuala muhimu ya jamii kutoka katika Barua ya Rerum Novarum, aliyeiendeleza kwa njia ya majisterio ya Roma na katika ushirika wao na maaskofu. Ni kweli kwamba, masuala yanayohusu mambo ya jamii haya kuanza na barua hiyo, kwani Kanisa halijawahi kushindwa kutimiza hamu yake katika masuala ya jamii. Hata hivyo, Rerum Novarum inaonesha njia mpya inayotokana na mapokeo ya mamia ya miaka iliyopita, ni alama ya mwanzo mpya na jambo moja la maendeleo ya kanisa katika maeneo ya jamii. Matukio ya mapinduzi ya viwanda yalileta changamoto la aina yake, kila aina ya kudharauliwa utu wa mwanadamu ilijitokeza, kujali zaidi faida ilikuwa kipaumbele ya uzalishaji. Kumbe hali hii ileta pia changamoto kwa kanisa na hivyo kutafuta njia sahihi ya kulihusisha hali hiyo na mafundisho yake. Kuchuja na kuelekeza nini kifanyike ili hali ya mwanadamu iendelee kuthaminiwa. Ndiyo maana Rerum Novarum ilichambua hali ya wafanyakazi wa mishahara na kwa namna ya pekee iliwalenga wale wanaofanyakazi viwandani ambao waliishi katika hali mbaya isiyo ya kiutu. Suala la wafanyakazi limezungumziwa kwa upana wake. Barua ilichambua masuala ya kijamii na kisiasa ili kuruhusu tathmini kufanyika katika mwanga wa kanuni zilizo katika msingi wa Ufunuo wa Mungu na sheria ya asili na uadilifu. Mafundisho hayo yalizingatia kuhusu kazi, haki ya mali, ushirikiano badala ya mapambano ya jamii, haki za wanyonge, heshima kwa maskini na wajibu wa tajiri, ukamilifu kuhusu haki kwa njia ya mapendo, haki ya kuunda vikundi vya wanataalamu. Ni katika barua hii kanisa liliweka bayana haki ya msingi ya mwanadamu, ile haki ya kuzaliwa nayo, na kwamba haki ya mwanadamu haitegemei aina fulani ya mfumo wa kisiasa, kiuchumi au ya kiutawala. Pia kanisa liliwaalika waana wake kuhuisha na kuiishi dhamiri njema kwa ajili ya maendeleo ya jamii nzima na pia kwa ajili ya uhusiano wao na Mwenyezi Mungu. Ni miaka zaidi ya mia yamepita, ujumbe wa mama Kanisa bado una hadhi ile ile, kwa wanajamii, wafanyakazi, wanasiasa, watawala, wanauchumi na wote wenye mapenzi mema. Kutenda kwa haki, upendo na kuwajali maskini na wenye shida bado ni kilio cha mama kanisa. Tukiangalia katika nchi zote duniani, zilizoendelea na zinazoendelea na hasa bara letu la Afrika, mama kanisa analo la kutuambia na sisi tunapaswa kusikiliza na kuiishi. Hali ya wafanyakazi, wakulima, wafanyabiashara, wanasiasa na wanajamii kwa ujumla wake bado haki inakosekana, amani iko matatani, uelewana hakuna, ugomvi na mapigano na wimbo wa kila siku. Na kwa sababu hiyo basi, tunadhiriki kusema kwamba mafundisho ya kanisa ni Biblia ya Waafrika, kwa sababu katika mafundisho kanisa imefafanuliwa na kuelekezwa namna nzuri ya kuishi mafundisho ya Kristu yaliyopo katika Biblia iliyo Neno lake. Ni katika mafundisho ya kanisa kuhusu jamii tunaweza kuyatambua matatizo yetu na hasa namna ya kuyatatua. Kwani katika mafundisho hayo tunaona na kuelekezwa namna ya kuuheshimu utu wa mwanadamu, kuheshimiana, upatanisho, kuunda jamii yenye haki na uelewana na yenye kutimiza mapenzi ya Mwenyezi Mungu. Kwa hakika ni mafundisho yasiyoweza kuzeeka na yanayomfaa kila mmoja mwenye mapenzi mema. Kumbe tuyathamini na kuyakumbatia mafundisho hayo. Hadi hapo tumefikia mwisho wa makala yetu ya leo, tukutane tena wiki ijayo siku na wakati kama huu, nikiwaaga kutoka studio ya radio vatikani Ni mimi Padre Nicodemus Hindoy OfmCap. Toka chuo kikuu cha kipapa cha Laterano - Roma
|