14/12/2010 8.37.16


Ujenzi wa misingi ya amani ni dhamana fungamanishi


|

Tume ya haki na amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani, hivi karibuni ilifanya mkutano uliopembua kwa kina na mapana kuhusu vita na amani. Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani ni kati ya wageni mashuhuri waliokuwa wamealika kutoa mada katika mkutano huo. Anasema, Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema, wanaalikwa na kuhimizwa kuwa ni wajenzi wa utamaduni wa amani, kwani madhara ya vita yanaendelea kujionesha sehemu mbali mbali za dunia.
Ikumbukwe kwamba, vita si sehemu ya vinasaba vya maisha ya mwanadamu. Amani na vita ni dhana inayopata chimbuko lake katika moyo wa mwanadamu. Umuhimu wa kukuza na kudumisha amani ni changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema. Vita ni matokeo ya uvunjifu wa misingi ya haki na uhuru; myumbo wa uchumi wa kimataifa na madhara ya mabadiliko ya tabianchi. Udumishaji wa amani ni wajibu fungamanishi na ni kwa ajili ya mafao ya wengi anasema Kardinali Turkson.
Hata baada ya kutoweka kwa vita baridi, bado Jumuiya ya Kimataifa inawajibu wa kulinda na kukuza misingi ya utamaduni wa amani, kwani kuna matukio ambayo yanaendelea kutishia amani duniani. Kardinali Turkson anasema bado kuna mataifa yanayoendelea kutengeneza na kuhifadhi silaha ya kinyuklia ambazo zimekuwa ni tishio kubwa la amani na usalama wa Jumuiya ya Kimataifa. Mashambulizi ya kigaidi kwa miaka ya hivi karibuni, yametikisa misingi ya amani na utulivu sehemu mbali mbali za dunia. Kinzani za kitamaduni, kisiasa, kikabila, kijamii; dhuluma na nyanyaso, yote haya ni matukio yanayohatarisha amani.
Kardinali Turkson anafafanua kwamba, dhana ya vita kadiri ya vyombo vingi vya habari za kijamii, ni jambo ambalo halitishi wala kuacha ukakasi katika maisha ya watu, lakini ikumbukwe kwamba, binadamu anachangamotishwa kumwilisha upendo katika maisha yake kwa kuondokana na falsafa ya kutumia mtutu wa bunduki kama suluhu ya migogoro inayomkabili mwanadamu. Hasira, chuki na hali ya kulipizana kisasi ni vyanzo vya vita na madhara yake katika maisha ya mwanadamu.
Kanisa Katoliki katika Mafundisho yake Jamii linafafanua kwamba, amani ni kielelezo cha utu wa mtu unaofumbata: ukweli, uhuru, haki na upendo. Amani ni fadhila inayomuunganisha mwanadamu na Muumba wake. Amani ni kigezo kikuu cha maendeleo na kielelezo cha mshikamano. Ni fadhila inayozingatia na kukumbatia tamaduni, maadili na maendeleo endelevu; bila kusahau utunzaji wa mazingira kama ushiriki mkamilifu wa kazi ya uumbaji. Ni ufafanuzi unaotolewa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita.
Kardinali Turkson anasema, viongozi wa dini wanao wajibu wa kimaadili kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na utulivu; kwa kujenga na kuimarisha jukwaa litakalojadili haki na upatanisho. Mwaka 2011, Kanisa Katoliki linaadhimisha Jubilee ya Miaka ishirini na mitano, tangu Hayati Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa pili, kunako mwaka 1986, alipoitisha mkutano wa viongozi wa dini mbali mbali kukutana mjini Assis kusali kwa pamoja na kujadili dhamana ya viongozi katika kudumisha misingi ya haki na amani.
Tume za haki na amani zilizoundwa kwenye baadhi ya nchi zimekuwa ni Jukwaa la kujadili kwa kina na mapana jinsi ya kutibu madonda na majeraha ya vita, chuki na ubaguzi wa rangi. Yote hii inaonesha kwamba, mwanadamu ana kiu ya kuona amani ikitawala katika mioyo ya watu. Hizi ni jitihada za mtu mmoja mmoja na Jamii kwa ujumla, katika ujenzi wa utamaduni wa amani. Jambo hili linawezekana anasema Kardinali Peter Turkson kwa kukuza na kudumisha misingi ya majadiliano na utamadunisho wa tunu msingi za maisha ya kijamii na kiutu. Kwa njia hii, upendo wa Mungu unaweza kuota mizizi kwa kumwilishwa katika maisha ya kila siku.
|