06/12/2010 9.02.31


Ushirika wa wakulima wa Zabibu, Dodoma ni njia muafaka itakayokoleza mapambano dhidi ya baa la umaskini


|

Zao la Zabibu linalolimwa kwa wingi mkoani Dodoma, likipewa msukumo wa pekee kwa kuongeza tija na uzalishaji, linaweza kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo na mapambano dhidi ya baa la umaskini miongoni mwa wakulima wa Zabibu, na hivyo kuufanya wimbo huu kuwa ni sehemu ya historia iliyopita kwa wananchi wa Mkoa wa Dodoma. Wakulima wengi walianza kukata tamaa kutokana na ukosefu wa soko la uhakika la Zabibu pamoja na uzalishaji hafifu, usiokidhi viwango.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na Padre Sebastian Mwaja, Paroko wa Parokia ya Mbabala, Jimbo Katoliki la Dodoma, wakati akizungumza na viongozi wa Shirika la Misaada la Kimataifa la Kanisa la Kiinjili la Kiluteri, kutoka Marekani walipotembelea Parokiani hapo kuangalia juhudi za uzalishaji wa zao la Zabibu kama sehemu ya pambano dhidi ya baa la umaskini. Ujumbe wa Shirika hili la Misaada kutoka Marekani, unaoongozwa na Dr. Evarist Kalangwa, pamoja na mambo mengine, unaangalia uwezekano wa kukuza na kuimarisha soko la Zabibu toka mkoani Dodoma.
Wakulima wa Zabibu mkoani Dodoma wanaweza kuutokomeza umaskini kwa kuungana na hivyo kuunda vyama vya Ushirika vitakavyokuwa na jukumu la kuwahakikishia uhakika wa soko; upatikanaji wa mitaji na pembejeo za kilimo kwa wakati muafaka.
Dr. Kalangwa anasema, Shirika lake, liko tayari kushirikiana na wakulima wa Zabibu kutoka Dodoma, ikiwa kama watashirikiana na kuunda Umoja wa Wakulima wa Zabibu ili kuunganisha sauti badala ya mwelekeo wa sasa kila mtu akijipigania mwenyewe kwa ajili ya masilahi yake binafsi. Kwa kufanya hivi, Shirika hili linaweza kuwapatia utaalam pamoja na kuwawezesha kwa mitaji.
|