HomeRadio Vaticana
foto testata  

Categories


  Charity & Solidarity


  Church


  Culture & Society


  Vatican Documents


  Synod


  Ecumenism


  Family


  Youth


  Justice & Peace


  Politics


  Religion & Dialogue


  Science & Ethics


  Audiences
   & Angelus



  Pastoral visits


cx_t01

CTV - You tube

CTV

 home > Charity & Solidarity  > news


25/10/2010 10.10.26



Muujiza wa ushirikiano wa kimissionari katika kumwilisha upendo wa Mungu kati ya watu maskini!






Padre Vincenti Boselli wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, amewashukuru kwa namna ya pekee waamini wa Parokia ya Bagnolo mella, Jimbo Katoliki la Brescia kwa ari, moyo na upendo, udugu na mshikamano wa kimissionari ambao wameuonesha kwa wananchi wa Tanzania kwa takribani miaka ishirini iliyopita, walipoanza kushirikiana nao katika kupambana na umaskini, magonjwa na ujinga hasa katika mikoa ya Singida, Dodoma na Morogoro.

Padre Boselli ameyasema hayo katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka ishirini tangu Kikundi cha Marafiki wa Wamissionari kilipoanzishwa rasmi huko Bagnolomella, Jimbo Katoliki la Brescia, Kaskazini mwa Italia kwa ajili ya kusaidia juhudi za kimissionari nchini Tanzania na Afrika ya Kati, sherehe ambazo zilikwenda sambamba na maadhimisho ya Siku ya themanini na nne ya umissionari duniani na kwa waamini wa Parokia ya Bagnolomella, walikuwa wanafanya kumbu kumbu ya kutabarukiwa kwa Kanisa lao.

Katika kipindi cha miaka kumi, (1990 - 2000) Kikundi hiki kinachowaunganisha waamini wa Parokia ya Bagonolomella, kimefanikiwa kujenga: Chuo cha Ufundi kwa Wasichana Manyoni, mahali ambapo wasichana kutoka mkoa wa Singida na Dodoma wamefaulu kupata maarifa na hatimaye, kuboresha maisha yao kwa njia ya ajira binafsi. Chuo hiki kilipanuliwa na kwa sasa ni shule ya Sekondari ya wasichana inayoleta matumaini makubwa kwa wasichana kutoka Kanda ya Kati.

Baadhi ya wasichana waliohitimu mafunzo yao ya ufundi walimejiendeleza na kwa sasa ni kati ya wakufunzi wanaotumainia katika vyuo vya ufundi nchini Tanzania. Baadhi ya wasichana walipata wito wa kujitoa kwa ajili ya Mungu na jirani zao na kwa sasa ni watawa wa Shirika la Masista Waabuduo Damu Azizi ya Kristo na Mashirika mengine nchini Tanzania.

Marafiki wa Wamissionari walijenga na kuboresha Zahanati kwa ajili ya Kijiji cha Wagonjwa wa Ukoma, Sukamahela, kilichoko Wilayani, Manyoni, Mkoani Singida, ili kuhakikisha kwamba, waathirika wa ugonjwa wa Ukoma kwanza kabisa wanaheshimiwa na kuthaminiwa kama binadamu na pili wanapata tiba kwa ugonjwa wao, ili waweze kuchangia maendeleo yao na ya taifa kwa ujumla.

Kikundi hiki, katika miaka yake kumi ya kwanza, kilijenga pia Maktaba ya Parokia ya Manyoni, mahali ambapo palipania kuwa ni kitovu cha maendeleo ya elimu, kwa kutoa nafasi kwa vijana na wazee kukutana kwa ajili ya majiundo endelevu kiroho na kimwili na ikawa pia ni sehemu ya mikutano kwa waamini na wananchi kwa ujumla. Ujenzi wa Maktaba anasema Padre Vincenti Boselli ulikwenda sanjari na upanuzi wa Kanisa la Parokia ya Kupaa Bwana Manyoni, ili kukidhi mahitaji ya ongezeko la waamini katika mji wa Manyoni.

Kutokana na ukosefu wa huduma bora ya afya, Kikundi hiki, kilianzisha Kituo cha Afya cha Maria De Mattias, ambacho kimekuwa ni msaada mkubwa kwa waanchi wa Wilaya ya Manyoni na vitongoji vyake kutokana na huduma safi inayotolewa na Masista Waabuduo Damu Azizi ya Kristo. Ni kimbilio la watu maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na umaskini wao.

Padre Vincenti Boselli anasema, kuanzia mwaka 2000 hadi 2010 Kikundi cha Marafiki wa Wamissionari kiliendelea kuimarisha juhudi za kusaidia mchakato wa kuleta maendeleo katika kazi za kimissionari nchini Tanzania kwa kusaidia tena ujenzi wa Kanisa la hija, "Mwili na Damu Takatifu Ya Yesu", lililopo mlima, Kola, Jimbo Katoliki la Morogoro, linalohudumiwa na Wamissionari wa Damu Azizi ya Kristo, Tanzania.

Shida, nyanyaso na unyanyapaa waliokuwa wanakabiliana nao watoto yatima na waliokuwa wameaathirika kwa virusi vya Ukimwi, kuliwafanya Wamissionari wa Damu Takatifu ya Yesu, Masista Waabuduo Damu Azizi ya Kristo pamoja na Kikundi cha Marafiki wa Wamissionari kwa pamoja kujitahidi kujibu "kilio cha damu" kutoka kwa watoto hawa, ndoto ambayo leo hii imezaa muujiza wa Kijiji cha Matumaini, Jimbo Katoliki la Dodoma, mahali ambapo watoto wanapata tiba ya kurefusha maisha, wanaonja upendo wa familia na majirani pamoja na kupata huduma ya elimu.

Kikundi hiki kwa njia ya majitoleo yao ya fedha, uwepo na mchango wao wa nguvu kazi, walifanikiwa kujenga kituo cha Afya kwa ajili ya kutoa tiba kwa watoto waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi ambao walikuwa pia ni yatima kutoka katika mikoa ya Dodoma, Singida na Morogoro. Kijiji cha Matumaini kwa sasa kina jumla ya watoto yatima na ambao wameaathirika kwa ugonjwa wa Ukimwi 160 wanaotunzwa na kulelewa katika mazingira ya kifamilia. Zaidi ya watu 2500 kutoka nje wanatibiwa magonya nyemelezi pamoja na kupata huduma za dawa ya kurefusha maisha.

Wamejenga na kuboresha maabara kwa ajili ya vipimo vya virusi vya Ukimwi, ili kutoa tiba ya uhakika zaidi pamoja na kuanzisha Kliniki kwa ajili ya Wanawake wajawazito, ili waweze kujifungua salam kama sehemu ya mkakati wa kupunguza maambukizi ya virusi vya ukimwi kutoka kwa Mama kwenda kwa mtoto, zoezi ambalo linaendelea kuonesha mafanikio makubwa.

Kikundi hiki kutoka Bagnolomella, Brescia, kilijenga pia Chekechea kwa ajili ya watoto wa Kijiji cha Matumaini na baadaye wakajenga, shule ya msingi inayohudumia watoto 490 wanaotoka vitongoji vilivyoko karibu na Kijiji cha Matumaini. Mwaka 2009 watoto wa Kijiji cha Matumaini walihitimu elimu ya msingi na kufaulu vizuri sana, jambo lililowapatia changamoto ya kujenga shule ya Sekondari na kwa sasa kuna wanafunzi wanaoendelea kusoma kidato cha kwanza.

Padre Vincento Boselli, muasisi wa Kijiji cha Matumaini anasema, changamoto wanayokabiliana nayo kwa sasa ni kuendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa bweni kwa wanafunzi wapatao 500. Lengo ni kuhakikisha kwamba, kadiri ya mapenzi ya Mungu, vijana hao ambao wamekuwa na kulelewa kwenye Kijiji cha Matumaini kama watoto yatima na waathirika wanapata matumaini katika maisha, ili baadaye, wao pia waweze kuwasaidia wadogo zao kama waalimu na wahudumu katika sekta mbali mbali za maisha ndani na nje ya Kijiji cha Matumaini.

Kwa ufupi Padre Boselli katika mahojiano na Radio Vatican anasema, huu ndio muujiza wa ushirikiano wa kimissionari uliowezesha upendo wa Mungu kumwilishwa kati ya watu maskini. Ninakualika kwa heshima na taadhima kumsikiliza Padre Boselli katika mahojiano haya:


  « back to index

 




















Related categories


Page précédente  Previous page
Page d'accueil  Home Page
Ecrire à la rédaction  Contact us
top
top
All the contents on this site are copyrighted ©. Webmaster / Credits / Legal Conditions
top
top