26/08/2010 8.01.23


Onyo:Maadhimisho ya Mwaka wa Vijana, Kisiwe ni Kipindi cha kukumbatia utamaduni wa kifo!


|

Inasikitisha kusikia kwamba, Maadhimisho ya Mwaka wa Vijana Kimataifa yameanza kwa mikiki mikiki ya kongamano linalopania kukumbatia utamaduni wa kifo kwa kuwajengea vijana dhana ya utoaji mimba katika maisha yao, kama kielelezo cha uhuru, kwa kisingizio cha afya ya uzazi, lugha ambayo kimsingi inafumbata sera za utoaji mimba.
Kwa bahati mbaya, hakuna mahali ambapo mkazo umewekwa ili kuonesha uhusiano wa dhati kati ya watoto na wazazi wao katika masuala ya mahusiano ya kijinsia. Padre Flavian Kassala Matindi katika makala ya vijana, anachambua kwa undani zaidi dira na mwelekeo wa maadhimisho ya Mwaka wa Vijana Kimataifa.
Mpendwa kijana, karibu katika makala yetu ya leo. Mapema mwezi huu, Umoja wa Mataifa umekitangaza kipindi cha mwaka mmoja, Agosti 2010 hadi Agosti 2011, kuwa kipindi maalum cha mwaka wa vijana.
Katika taarifa yake, Umoja wa Mataifa umesisitiza kutumika kwa kipindi hiki katika kujenga mahusiano ya karibu baina ya vijana wa nyanja mbalimbali duniani.Maadhimisho haya ya mwaka vijana yanaambatana na kuandaliwa kwa kongamano maalum la kujadili hali ya vijana na kuweka mikakati kwa ajili ya kuboresha hali ya vijana duniani. Kongamano hili limeanza mapema wiki hii huko nchini Mexico.
Miongoni mwa maazimio ya kongamano hili la vijana ni kuangalia hali ya takribani asilimia 87 ya vijana katika nchi zinazoendelea ambao wameathirika kwa kiasi kikubwa sana na kuyumba kwa uchumi duniani. Azimio hili linakwenda sambamba na jitihada za kudumisha amani, heshima kwa haki za binadamu na mshikamano. Hali ya ongezeko wa watu duniani pia imetajwa kuwa moja wapo ya maazimio ya mwaka huu wa vijana.
Yakiwa katika hatua zake za mwanzo kabisa, maadhimisho haya ya mwaka wa vijana yameonesha wasiwasi mkubwa hasa katika kujadili mbinu za kuiwezesha jamii kutekeleza maazimio muhimu yanayolenga katika kuboresha hali ya vijana duniani. Hii inatokana na msisitizo mkubwa unaotolewa katika ongezeko wa watu duniani kama tatizo msingi la hali duni ya vijana duniani. Kutokana na msisitizo huo, kumejitokeza mwegemeo mkubwa katika kutafuta jinsi ya kudhibiti ongozeko hili bila kuangalia hali halisi ya maadili ya kijamii na ya vijana.
Wakati hakuna msisitizo wowote katika nafasi ya familia kama mhimili wa kwanza katika kuwalea vijana, kongamano hili la vijana limeonesha wazi kuvutiwa na matumizi ya njia zinazokiuka haki za binadamu kama suruhisho la hali duni ya vijana. Hii inahusisha kampeni zinazoendelea za kuunga mkono utoaji mimba kama suruhisho kwa ongezeko la idadi ya watu duniani. Hatua hii inatishia kudidimiza zaidi hali ya vijana kimaadili, kijamii na hata kisaikolojia hata kama itawafanikisha kupata mafanikio fulani kiuchumi.
Makala yetu inaunga mkono juhudi zote za umoja wa mataifa katika kuhakikisha vijana wanapatiwa ufanisi mkubwa katika maisha yao, ikiwa ni pamoja na kuwahakikishia hali bora zaidi katika afya zao kimwili na kiakili. Hata hivyo inawaonya vijana kuwa chonjo na mapendekezo yote ya njia zinazotishia kuwafanya watumwa zaidi wa maendeleo hata kusahau hadhi yao ya ubinadamu.
Hii inahusisha pia kulinda na kuheshimu nafasi waliyonayo binadamu wenzetu, hasa wale walio dhaifu zaidi. Utoaji mimba hauwezi kuwa suruhu kwa matatizo ya vijana. Tunaendelea kusisitiza na kuwaalika wanaharakati wote wa mchakato huu kuirudishia familia hadhi yake ya kulea na kuongoza vijana katika makuzi yao. Hata kile kinachokimbiliwa kama afya ya uzazi hakiwezi kupatikana iwapo vijana hawatakipokea toka katika familia zao ambazo zinabaki kuwa mhimili wa kwanza kabisa wa malezi na makuzi kwa vijana.
Tunaushukuru Umoja wa Mataifa kwa zawadi hii ya mwaka wa vijana, lakini tunaomba uwe mwaka wa kutujenga zaidi kuliko kutusukuma katika maangamizo yetu. Kutoka Studio hizi la Radio Vatican ni mtumishi wa vijana, Padre Flavian Kassala.
|