17/08/2010 11.02.32


Jubilee ya miaka 50 ya uhuru wa Congo ilete mwamko wa kuboresha huduma za kijamii katika sekta ya elimu na afya


|

Baraza la Maaskofu Katoliki Congo, Brazaville wakati huu wa maadhimisho ya Jubilee ya Miaka hamsini tangu walipojinyakulia uhuru kutoka kwa mkoloni, wanawaalika waamini na wananchi wa Congo kwa ujumla, kufanya hija ya maisha ya kiroho kwa tafakari ya kina, kama alivyofanya Bikira Maria, ili waweze kusonga mbele kwa imani na matumaini, wakijikita zaidi katika harakati za kuwaletea wananchi mabadiliko mintarafu upendo na mshikamano, ili kutekeleza mikakati ya maendeleo katika sekta mbali mbali za maisha.
Twekeni hadi kilindini ndiyo kauli mbiu inayoongoza Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Congo, wakati huu wa maadhimisho ya Jubilee ya miaka hamsini tangu walipojinyakulia uhuru wao, tarehe 15 Agosti, 1960, Siku kuu ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho. Ndiyo maana Nchi ya Congo ikawekwa chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria Mpalizwa mbinguni, tukio lililofanywa na Rais wa kwanza kabisa wa Congo Fulbert Youlou. Hiki ni kielelezo thabiti kwamba, nchi hii ina mizizi yake katika fadhila na tunu msingi za maisha ya kikristo na Kiinjili.
Maaskofu wanasema, maadhimisho ya Jubilee ya miaka hamsini ya uhuru wa Congo si haba, kwani ni kipindi ambacho kimesheheni pia shida na magumu kwa wananchi wa Congo hasa kutokana na vita, changamoto ya kuondokana na falsafa hiyo iliyopitwa na wakati, ili hatimaye, kuomba msamaha na huruma ya Mungu na jirani, ili kuanza tena upya kwa kutweka katika Kristo.
Maaskofu wanasema, mapambano bado yanaendelea dhidi ya rushwa, ubadhirifu wa mali ya umma na ufisadi, dhambi zinazokwamisha juhudi za kuwaletea wananchi maendeleo endelevu. Maaskofu wanawatambua wananchi na kwamba, Kanisa Barani Afrika, daima limekuwa mstari wa mbele katika jitihada za kujenga msingi wa haki, amani na upatanisho, kama njia ya kuleta ufumbuzi wa matatizo ya kijamii yanayowasibu wananchi wa Bara la Afrika.
Bado kuna haja ya kujifunga kibwebwe katika harakati za kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi wa Congo hasa katika sekta ya elimu na afya katika ngazi mbali mbali. Huu ni wajibu wa kwanza kabisa kwa viongozi wa Serikali kwa kushirikiana na wadau mbali mbali, wanaopania kuboresha maisha ya wananchi wa Congo. Kanisa kwa upande wake, limekuwa nikitekeleza wajibu huu hata kabla ya kupata uhuru, linapenda kuendelea kujikita kutoa huduma za kijamii kwa ajili ya mafao ya wengi, ili kudumisha utu na heshima ya mwanadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Maaskofu wanasema, amani ya kweli inajengeka katika msingi wa amani, haki na upatanisho; kama kigezo cha maendeleo endelevu yanayozingatia mahitaji ya mtu mzima kiroho na kimwili; daima, yakiongozwa na kanuni ya mshikamano wa dhati. Huu ndio mwelekeo wa Mafundisho Jamii ya Kanisa, rejea makini katika ukweli, uhuru na mshikamano unaopania kudumisha mafao ya wengi na maisha ya mwanadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
|