13/08/2010 7.32.16


Shirika la Masista wa Huruma, Kilimanjaro na mikakati na changamoto za huduma za kijamii


|

Sr. Josephina Mushi, Mama Mkuu wa Shirika la Masista wa Bibi Yetu wa Kilimanjaro, lenye makao yake makuu Jimbo Katoliki la Moshi, Tanzania anaelezea changamoto wanazokabiliana nazo katika harakati ya utoaji huduma kwa wananchi wa Afrika Mashariki katika sekta ya elimu na afya, mintarafu karama ya Shirika lao; huduma wanayoitekeleza kwa kusoma pia alama za nyakati.
Kutokana na kuchechemea kwa uchumi wa kimataifa, Sr. Mushi anasema, wanakabiliana na changamoto ya kuhakikisha kwamba, wanadumisha kiwango bora cha huduma, lakini pia wakitafuta mbinu mbadala zitakazowawezesha kumudu kishindo cha gharama za uendeshaji wa shughuli hizi za kichungaji.
Kuna idadi kubwa ya watoto wanaotoka kwenye familia zenye uwezo mdogo kiuchumi na kundi kubwa la watoto yatima, ambao wote hawa kimsingi wanahitaji kupatiwa huduma ya elimu kama sehemu ya haki zao msingi.
Kama Shirika wakati mwingine wanashindwa kutekeleza changamoto hii, lakini, wanaendelea kufanya yote kwa sifa na utukufu wa Mungu, ili kuhakikisha kwamba, vijana wa kizazi hiki wanaokabiliwa na changamoto mbali mbali kutoka katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia wanapata walau msingi wa malezi bora, tangu mwanzo.
Ni jukumu linalopaswa kutekelezwa kwa ushirikiano mkubwa kati ya walimu, wazazi na walezi wa watoto husika. Tunajiunga na Sr. Josephina Mushi kwa ufafanuzi zaidi.
|