05/08/2010 13.52.17


Kura ya Maoni ya "Ndiyo" inaelekea kushinda nchini Kenya ili kupitisha muswada wa katiba Mpya!


|

Wachunguzi wa masuala ya kisiasa nchini Kenya wanasema kwamba, kuna dalili kwamba, wananchi wa Kenya wameamua kuunga mkono Muswada wa Katiba Mpya ya Kenya, licha ya kuonesha mapungufu katika masuala ya utoaji mimba na uhuru wa kidini, katika kura ya maoni iliyopigwa nchini humo hapo tarehe 4 Agosti, 2010.
Matokeo ya awali yanaonesha kwamba, asilimia 67% ya wapiga kura wote wanaunga mkono Muswada wa Katiba Mpya ya Kenya. Zaidi ya wapiga kura ya maoni millioni 12.4 walijiandikisha na kushiriki kupiga kura, ili kura ya "Ndiyo" iweze kupata ushindi, zaidi ya wananchi millioni 4.3 wakubaliane na Muswada huo.
Kura ya maoni imefanyika katika hali ya utulivu na amani katika sehemu mbali mbali za Kenya. Viongozi mbali mbali wa Kanisa wamepongeza hatua hii ya utulivu wakati wa mchakato mzima wa kupiga kura ya maoni, kwani hapo mwanzoni kulianza kuonesha wasi wasi ya fujo na vurugu.
Makanisa nchini Kenya, yaliendesha Kampeni kupinga muswada wa Katiba Mpya ya Kenya kutokana na baadhi ya vipengele kukumbatia utamaduni wa kifo kwa kuhalalisha utoaji mimba, jambo linalokwenda kinyume kabisa cha haki msingi za kibinadamu.
Ni jambo ambalo pia liliwahi kuzungumziwa na Rais Mwai Kibaki wa Kenya, wakati wa sherehe za kumsimika Askofu Maurice Muhatia Makumba wa Jimbo Katoliki la Nakuru. Rais KIbaki, binafsi alikuwa nakerwa na kipengele hiki kuingizwa katika muswada wa Katiba Mpya ya Kenya.
Licha ya ushindi wa Kura ya Ndiyo kwa muswada wa katiba Mpya ya Kenya, viongozi mbali mbali wa Makanisa nchini Kenya wanasema kwamba, wataendelea kuwa ni sauti ya kinabii katika masuala mbali mbali yanayogusa mafao ya wengi, utu na heshima ya mwanadamu, maadili na utu wema; bila kusahau haki, amani na upatanisho.
|