21/07/2010 10.55.01


Kanisa linajifunga kibwebwe kupambana na umaskini, ili kuwaletea watu maendeleo ya kweli!


|

Askofu Manuel Antonio Santos wa Jimbo la Sao Tome na Principe anasema kwamba, Kanisa linapaswa kujifunga kibwebwe kuhakikisha kwamba, linaendeleza utume wake wa kinabii katika mapambano dhidi ya baa la umaskini, kwa kuwapatia wananchi mbinu na mikakati itakayowasaidia kuondokana na umaskini, ili kujiletea maendeleo endelevu yanayogusa mahitaji msingi ya binadamu.
Ni changamoto ya kuwa mstari wa mbele kupiga vita mambo yote yanayosababisha umaskini miongoni mwa watu kwa kuhimiza misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano pamoja na kutumia kikamilifu rasilimali iliyopo kwa maendeleo ya watu wengi zaidi.
Uinjilishaji ambao ni kiini cha utume na maisha ya Mama Kanisa, unakwenda sambamba na utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu, ushuhuda wa maisha unaofumbatwa katika umoja na mshikamano, majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kutafuta mafao ya wengi ndani ya jamii, ushirikiano na wadau mbali mbali wanaopania kumhudumia mwanadamu, kwa kutoa kipaumbele kwa watu wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.
Askofu Santos ameyasema hayo hivi karibuni mara baada ya mkutano wa tisa, uliowajumuisha Maaskofu kutoka katika nchi ambazo zinazungumza lugha ya Kireno, waliokutana huko Sao Tome. Huu ni mkutano unaofanyika kila baada ya miaka miwili. Mkutano huu uliwakutanisha Maaskofu Katoliki kutoka Brazil, Angola, Cape Verde, Guinea Bissau, Msumbiji, Ureno, Sao Tome na Principe. Maaskofu hawa walikuwa wanajadili kwa kina jinsi ya kupambana na baa la umaskini duniani.
Watu wanataka maendeleo ya kweli kwa kupunguza umaskini pamoja na kuhakikisha mgawanyo sawa wa ardhi na rasilimali ya nchi. Wananchi wanapaswa kupinga kwa nguvu zao zote vitendo vyote vya kutoa na kupokea rushwa kwani vinapindisha haki msingi ndani ya jamii. Ubadhirifu wa mali ya umma, rushwa na ufisadi ni maadui wanaokwamisha mchakato wa maendeleo ya watu, vitendo ambavyo kamwe haviwezi kufumbiwa macho, ikiwa kama Bara la Afrika linahitaji kupata maendeleo ya kweli na kuondokana na baa la umaskini.
Mizizi ya umaskini inaweza kung'olewa ikiwa kama wananchi watawezeshwa kwa njia ya elimu bora, inayowapatia fursa ya kupambana vyema na mazingira yao, ili kujenga nchi yao iwe ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Sambamba na jambo hili uboreshaji wa huduma za afya kwa jamii pamoja na kutoa kipaumbele kwa haki ili iweze kushika mkondo wake.
Askofu Manuel Antonio Santos anasema, ikiwa kama Kanisa linasaidia juhudi za Serikali kupambana na umaskini, ujinga na maradhi, inapaswa pia kuliwezesha Kanisa kutekeleza dhamana hii kwa niaba ya Serikali yenyewe.
Itakumbukwa kwamba, Umoja wa Ulaya umetenga Mwaka 2010 kuwa mwaka wa mapambano dhidi ya baa la umaskini na ubaguzi wa kijamii, mada ambayo pia imejadiliwa kwa mapana na Maaskofu wanaotoka katika nchi zinazozungumza lugha ya Kireno wakati wa mkutano wao.
Kutokana na muda kuyoyoma kwa kasi, athari za mabadiliko ya tabia nchi, kuchechemea kwa uchumi wa kimataifa, vita na misigano mbali mbali, si rahisi kuweza kufikia Malengo ya Maendeleo ya Millenia ifikapo mwaka 2015. Pengo kati ya nchi maskini na tajiri duniani linazidi kuongezeka kwa kasi.
|