15/07/2010 13.15.35


Afrika ya Kusini inapaswa kuendeleza mchakato wa mageuzi kwa kutumia ujuzi na mang'amuzi ya Mashindano ya Kombe la Dunia


|

Kardinali Wilfrid Napier, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Durban, Afrika ya Kusini anasema, Afrika ya Kusini ni nchi ambayo iko kwenye mchakato wa mabadiliko yanayopania kuifanya iwe ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.
Mashindano ya Kombe la Dunia Afrika ya Kusini mwaka 2010, yamekuwa ni fursa makini kwa wananchi wa Afrika ya Kusini kufanya kazi kwa umoja na mshikamano na kuihakikishia Jumuiya ya Kimataifa kwamba, Afrika ya Kusini ni Taifa ambalo lina watu wenye uwezo wa kupanga na kutekeleza maamuzi yao.
Kardinali Napier anachukua fursa hii kuipongeza Serikali ya Afrika ya Kusini, Kamati ya Maandalizi ya Kombe la Dunia, watu waliojitolea, wajenzi na wafanyakazi, bila kuwasahau wote waliojihusisha kwa namna moja au nyingine kuchangia mafanikio yaliyofikiwa Afrika ya Kusini wakati wa Mashindano ya Kombe la Dunia, kwa mwaka 2010. Wananchi wanapaswa kuendeleza mafanikio haya na kuifanya Afrika ya Kusini kuwa ni kituo cha matukio ya kimataifa.
Kwa namna ya pekee analishukuru Jeshi la Polisi na Vikosi vyote vya ulinzi na usalama kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana, kwa kuhakikisha usalama kwa wageni wote waliofika Afrika ya Kusini kushuhudia kabumbu ya kimataifa ikitandazwa kwenye viwanja mbali mbali vya michezo nchini humo.
Afrika ya Kusini imeonesha uwezo mkubwa wa kufanya kazi, kujenga, kuratibu na kulinda. Umefika wakati kwa wananchi kutumia uwezo na uzoefu huu, ili kuhakikisha kwamba, unatumiwa kikamilifu katika kukabiliana na vipaumbele vya wananchi wa Afrika ya Kusini, yaani elimu bora, afya, mapambano dhidi ya makosa ya jinai pamoja na uboreshaji wa huduma zinazotolewa na Serikali kwa umma. Afrika ya Kusini imeonesha kwamba, jambo hili linawezekana, sasa kazi kwao!.
|