10/07/2010 13.56.54


Afrika ya Kusini yalaani picha inayomdhalilisha Mzee Nelson Mandela


|

Chama cha ANC cha Afrika ya Kusini kimelaani vikali picha iliyochorwa na msaniii mmoja nchini Afrika ya Kusini kwa kumwonesha Mzee Nelsoni Mandela, akiwa anafanyiwa uchunguzi kwenye chumba cha maiti katika moja ya Hospitali maarufu za Afrika ya Kusini, tukio ambalo linashuhudiwa na baadhi ya wanasiasa maarufu.
Taarifa ya ANC iliyotolewa Jumamosi, tarehe 10 Julai, 2010 inasema, picha hii inamvunjia heshima na kumdhalilisha Mzee Nelson Mandela na pia ni kinyume cha maadili na utu wema. Lakini msanii wa picha hii kutoka Afrika ya Kusini Yuill Damaso anajitetea na kusema kwamba, picha ya Mzee Mandela inalenga kumwonesha jinsi alivyo kama watu wengine wa kawaida licha ya mchango wake katika mapambano dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika ya Kusini, utendaji wake mahiri wa kazi na sifa kubwa aliyojijengea katika Jumuiya ya Kimataifa.
Mzee Nelson Mandela, maarufu sana Afrika ya Kusini kwa jina la Mzee Madiba, hapo tarehe 18 Julai, 2010 atakuwa anatimiza miaka tisini na mbili tangu alipozaliwa. Kwa siku za hivi karibuni amepunguza shughuli zake katika hadhara kutokana na hali ya afya yake na chumvi nyingi aliyokula katika maisha yake.
|